Quantcast
Channel: NYINGINE – ShaffihDauda
Viewing all 565 articles
Browse latest View live

TFF imemfungia kocha miaka 5 kujihusisha na soka

$
0
0

Kamati ya Maadili ya TFF iliyokutana Februari 3, 2018 na Februari 17, 2018, katika ofisi za TFF Karume, pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa pia ilipitia na kutoa hukumu ya tuhuma za kutoa taarifa zisizo sahihi na kughushi leseni za usajili zilizowakabili watuhumiwa mbalimbali walioletwa mbele yake.

Tuhuma hizo zilitokana na mechi namba 26 Kundi A ligi daraja la kwanza iliyofanyika Oktoba 29, 2017 kati ya Mvuvumwa FC na Friends Rangers ambapo katika mchezo huo timu ya Mvuvumwa FC iliwachezesha wachezaji watano (5) ambao ni Elias Costa Elias (jezi namba 5), Lukwesa Joseph Kanakamfumu (jezi namba 7), Dunia Abdallah Dunia (jezi namba 1), Doto Justine Kana (jezi namba 12) na Mwarami Abdala Mwarami (jezi namba 8).

Kamati imemtia hatiani kocha na mratibu wa Mvuvumwa FC Joseph Kanakamfumu kwa makosa yote mawili, kutoa taarifa zisizo sahihi, (udanganyifu) ili kufanikisha usajili wa wachezaji kinyume na taratibu za ligi daraja la kwanza.

Kosa la kwanza Kanakamfumu akiwa kocha wa Mvuvumwa FC aliwaorodhesha wachezaji (Elias Costa Elias, Lukwesa Joseph Kanakamfumu, Dunia Abdallah Dunia, Doto Justine Kana Mwarami Abdala Mwaram) kushiriki mechi namba 26 huku akijua kwamba hawana leseni halali kutoka TFF, wachezaji wote walitoka katika kituo ‘academy’ anayoiendesha hivyo ni dhahiri alijua alichokuwa anakifanya.

Kosa la pili Kanakamfumu aliamua kuwaongeza wachezaji hao baada ya kukabidhiwa timu kwa vile alifahamu uwezo wao na inaonekana alitumia uzoefu wake katika mpira wa miguu kupata leseni za kughushi.

Kwa makosa hayo, kamati inamfungia Joseph Kanakamfumu kutojihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi cha miaka mitano.


Mafanikio ya Msuva yanapogeuka changamoto kwa mdogo wake

$
0
0

James Msuva ni mdogo wake Simon Msuva ambaye kwa sasa anakipiga kwenye klabu ya Difaa el Jadida ya Morocco, james ni miongoni mwa wachezaji wa mbao ambao wanafanya vizuri kwa sasa tofauti na wakati alipojiunga na klabu hiyo ya Mwanza ambapo alikuwa anaanzia benchi lakini siku za hivi karibuni amekuwa miongoni mwa wachezaji wanaounda kikosi cha kwanza.

James ameelezea changamoto mbalimbali anazokabiliana nazo kwenye soka la Tanzania ili kufikia malengo yake pengine hata pale alipofikia kaka yake.

“Namshukuru Mungu toka nilipotoka hadi nilipo sasa hivi, kuna mabadiliko makubwa ambayo nimeyaona hususan nilivyojengwa kiakili na kimwili, kumenibadilisha kwa namna moja ama nyingine kwa sababu ligi yetu ya Tanzania inachangamoto nyingi kama usipokuwa na utimamu wa mwili na akili huwezi kucheza.”

“Namshukuru mwalimu wangu (Etiene Ndayiragije) na uongozi wa Mbao kwa kukiona kipaji changu na kukibadilisha, waliamini kwamba James huyu waliyenaye kipindi fulani akiendelezwa na aka-focus atabadilika.”

“Kwa sasa kuna maendeleo mengi kwa sababu nilivyokuwa mwanzo ni tofauti na nilivyo sasa, napambana na najitoa ukizingatia kuna ndugu yangu (Simon Msuva) ambaye ameshatoka Tanzania na nilikuwa naona changamoto nyingi wakati anahaingaika na kupambana kabla ya mechi zake, vitu vyote hivyo nilivichukua kama changamoto kwangu na sehemu ya kujifunza.”

James ametaja baadhi ya vitu ambavyo anajifunza kutoka kwa kaka yake kuelekea kwenye mafanikio katika soka.

“Uvumilivu, alivumilia sana kwa sababu alikutana na mambo mengi kama matusi, fedheha  na maneno mengi lakini aliamua kuvumilia akimini hii ni safari ndefu na haiishii Tanzania na ipo siku atafika anapotaka na kweli amesogea, hivyo ni vitu ambavyo najifunza kutoka kwake.”

Unaambiwa kuwa James Msuva anapata changamoto kubwa kutokana na kaka yake kufanya vizuri nje ya mipaka ya Tanzania kwa sababu watu wengi wamekuwa wakiwalinganisha.

“Nina deni kubwa sana hasa kipindi ambacho anafanya vizuri kwa kufunga. Kwa kweli ananipa changamoto kubwa sana kwa sababu watanzania tunatabia ya kulinganisha mambo, kwa mfano mtu anaweza akahoji kwa nini mimi sifanyi mambo ambayo yanafanywa na Simon wakati huo anasahau ilimchukua miaka mingi hadi kufika hapo. Halafu mimi nina njia zangu siwezi jua nitafika vipi alipo yeye lakini naelewa kujituma na uvumilivu ndiyo kutanifikisha huko.”

James anaamini anaweza kufikia malengo yake ya kucheza nje ya nchi bila kupita kwenye vilabu vikubwa vya Tanzania endapo tu atafanya vizuri kwenye klabu anayoitumikia lakini ikitokea vilabu hivyo vikamuhitaji atakwenda kufanya kazi.

“Mpira ni malengo lakini pia kuna watu wanakuangalia zaidi ya wewe unavyojitazama, mimi natamani sana nicheze mpira nje ya hapa lakini kuna kitu kinaitwa changamoto, kakaangu kila siku ananisisitiza nitengeneze kwanza ndani licha ya mimi kutamani kucheza nje. Kwa hiyo naamini nikikomaa hapa nitafikia malengo, siwezi kusema natamani kucheza Simba, Yanga au Azam nipo tayari kucheza timu yoyote itakayovutiwa na mimi.”

Rage navyomkumbuka mchezaji wa Simba aliyefariki

$
0
0

Kiungo wa zamani wa Sunderland na baadaye Simba Arthur Mambeta amefariki dunia jana Alhamisi Februari 28, 2018. Mambeta si jina geni katika ramani ya soka la Tanzania, ni miongoni mwa wachezaji waliosaidia maendelo na kukua kwa mpira wa nchi hii.

Mwenyekiti wa zamani wa simba Alhaj Aden Rage ameeleza namna ambavyo anamkumbuka Arthur Mambeta pamoja na kuuomba uongozi wa Simba kushiriki kikamilifu katika msiba huo kwa ajili ya heshima ya klabu yao.

“Mambeta ni mchezaji ambaye ana sifa ya pekee ndani ya klabu ya Sunderland mpaka Simba, hakuteteleka wala hakuwa na kuhangaika kwa kuhama kwenda timu nyingine, maisha yake yote amechezea Sunderland na baadaye Simba kabla ya kustaafu akiwa Simba.”

“Kitu ambacho tutaendelea kumkumbuka Mambeta mwaka 1973 yeye ndiye aliyeongoza kikosi cha Simba ambacho Haidary Abeid Muchacho alifunga goli moja na kuondoa utawala uliokuwa wa Yanaga uliokuwa umedumu kwa muda mrefu sana.”

“Kwa wakazi wa Tabora, alikuwa mchezaji wa Railway Training School hapa sisi tukiwa wadogo kabisa alikuwa ni mchezaji hodari sana wakati anasoma.”

“Nawaomba viongozi wangu wa Simba, kwakuwa huyu alikuwa mchezaji mwenye nidhamu na mapenzi makubwa kwa klabu na alipata madhara makubwa kabla ya kufariki kwa kukatwa miguu yote miwili kwa sababu alikuwa anaumwa. Naomba uongozi wa Simba huu msiba uwahusu wao na ikiwezekana waende Kigamboni kushiriki kikamilifu kumsitiri mchezaji wetu kwa heshima za klabu yetu ya Simba.

Mdogo wake Arthur Mambeta anayefahamika kwa jina la Steven Mambeta amethibitisha kufariki kwa kaka yake jana saa 12 jioni.

“Taarifa ni kwamba, alifariki jana saa 12 jioni, mwili wa marehemu upo hospitali ya Temeke lakini msiba upo Kibugumo, Darajani-Kigamboni.”

Vilabu vimepewa darasa kujiendesha kwa faida

$
0
0

Semina ya siku moja yenye lengo la kuvijengea uwezo vilabu vinavyoshiriki ligi kuu, ligi daraja la kwanza na la pili imefanyika leo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali walioviwakilisha vilabu hivyo.

Semina hiyo imefunguliwa na Rais wa TFF Wallace Karia ambayo imeandaliwa na kampuni ya ISDI na kuwezeshwa na Alliance Life Insurance ina lengo la kuvijengea uwezo vilabu ili kujiendesha kwa mfumo wa kisasa wa kibiashara.

Mwenyekiti wa ISDI Dr. Katunzi amezungumzia malengo ya kuandaa semina hiyo kwa ajili ya kusaidia kutoa elimu kwa vilabu vya soka nchini kujiendesha kwa faida.

“ISDI iliangalia mchango wa michezo katika ukuaji wa uchumi vilevile chanagamoto ambazo michezo inakabiliwa nayo kwa hiyo ISDI kwanza tunafanya tafiti kubaini matatizo halafu tuna-link yale matatizo katika kujenga uwezo na sasa ISDI tumeanza na mpira wa miguu lakini si mpira wamiguu peke yake, tunaangalia michezo yote pamoja na utamatuduni.”

“Serikali ina nafasi yake kwenye kitu tunachokifanya, ISDI inategemea sana ushirikiano kutoka kwa vyombo vinavyoongoza michezo husika pamoja na serikali kwa ujumla. ISDI tumepata ushirikiano mkubwa toka TFF na bodi ya ligi kwa hiyo tunawashukuru kwa kuonesha utayari wa kushirikiana na sisi na tunategemea malengo ya semina hii yataleta chachu katika utendaji wa klabu zinazoshiriki ligi mbalimbali.”

Kwa upande wa shirikisho la soka Tanzania (TFF) limesema, halitaruhusu ligi kuu kuanza msimu ujao endapo timu shiriki hazitakuwa zimewakatia bima wachezaji wake pamoja na benchi la ufundi.

Rais wa TFF Wallace Karia ametoa kauli hiyo wakati akifungua semina ya uendeshaji wa vilabu kwa faida.

Wamefanya tafiti na wanaendelea kufanya tafiti ambazo zitatusaidia kuangalia jinsi gani hivi vilabu vinaweza kuendeshwa kwa ufanisi zaidi ambao tunauhitaji hasa wa kiuchumi ambao utatusaidia katika club licensing.”

“Vilabu vilivyopo hapa vya ligi kuu, daraja la kwanza na daraja la pili ndio ligi zinazoshirikisha timu nyingi ambazo zinatoka karibu kila mkoa, kwa hiyo zitakapoendeshwa kitaaluma zaidi zitatusaidia na sisi kuwa na mipango mikakati.”

“Nitoe wito kwa wadau wengine wote ambao wanaona wana kitu wanaweza wakafanya kwa kushirikiana na sisi niwaambie TFF iko salama.”

Dr. Jonas Tiboroha ambaye ni director wa ISDI ameelezea kwa kifupi namna watakavyovisaidia vilabu kujiendesha kwa faida.

“Kwenye mpango mkakati wetu wa mwaka 2018-2022 kwa maana ya miaka mitano ijayo, tunayo ‘strategic research agenda’, agenda yetu kubwa ni kwenye transformation of sport kuwa tool ya job creation na poverty alleviation.”“

“Kitu tunachokiongea hapa ni kuhakikisha tunayapa kipaumbele hayo mambo na ukijaribu kuangalia mjadala wetu wa leo kutokana na utafiti ambao tumeufanya na kupata majibu, tunajaribu kuangalia ni namna gani vilabu vinaweza kuendeshwa kwa faida au kwa uwezo mzuri kiasi kwamba program za maendelo zinaweza kupelekea vijana kuja kuajiliwa kwenye mpira wa miguu zifanikiwe.”

Mo kamtibua kocha

$
0
0

Kocha mkuu wa Simba Pierre Lechantre ameweka wazi sababu za mchezaji Mohamed Ibrahim ‘Mo’ kutoonekana hata kwenye orodha ya wachezaji wa akiba baada ya ujio wake ndani ya kikosi cha wekundu wa Msimbazi.

“Nina matatizo na Mo kwa sababu unajua timu ya mpira ni kama jeshi, anadhani Simba ni kama klabu ya kujiachia, anakuja mazoezini anavyotaka akija leo kesho haji. Anasema mkewe kapata mtoto au anasubiri mtoto, siwezi kukubaliana na hiki kitu.”

“Tunapaswa kuwa na weledi zaidi ndani ya klabu hii, mchezaji wako asipokuja mara ya kwanza ya pili na ya tatu sikubaliani na vitu hivi. Ally Shomari nafikiri anasumbuliwa na Malaria.”

Mo amekosa nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Simba tangu Joseph Omog akiwa kocha mkuu lakini baada ya ujio wa lichantre amekuwa haonekani hata kwenye benchi yeye pamoja na Juma Liuzio.

Kocha aliyefungiwa miaka 5 amekata rufaa

$
0
0

Baada ya kuhukumiwa miaka mitano kutojihisha na masuala ya soka, kocha Joseph Kanakamfumu ameamua kukata rufaa juu ya hukumu hiyo iliyotolewa na kamati ya maadili ya TFF baada ya kumtia hatiani katika makosa ya kutoa taarifa zisizo sahihi na kughusi leseni za usajili wa wachezaji.

Emanuel Muga ambaye ni wakili wa Kanakamfumu amesema amebaini sababu tano nzito za kukata rufaa huku akiwa na matumaini mteja wake atashinda katika rufaa hiyo.

“Amenipa maelekezo kwamba, nimsaiie kukata rufaa dhidi ya hukumu iliyotolewa na kamati ya maadili kwa hiyo tumeshachukua hatua kadhaa hadi sasa, tumeomba nakala ya hukumu ya kina kwa sababu kanuni za maadili za TFF zinasema ili ukate rufaa lazima upewe nakala ya hukumu. Ukishapewa siku za kukata rufaa zinaanza kuhesabiwa ambazo ni siku tatu, hivyo tukishapewa hiyo nakala siku tatu zitaanza kuhesabika na hapo ndio tutakata rufaa.”

“Vyombo vya habari vimeripoti kwamba, Kanakamfumu amefungiwa na pia imezoeleka kwamba kila kamati ikitoa maamuzi yake basi mtu anaanza kufungiwa hapohapo lakini si kweli, kanuni za maadili zinasema kwamba akishafahamishwa kuhusu uamuzi ndio adhabu inaanza, sasa mtu anafahamisha uamuzi kupitia njia mbili tu ambazo zimetajwa na kanuni njia ya kwanza ni fax na nyingine ni registered letter ‘barua iliyopitia posta lakini imekuja kwa register’.”

“Joseph Kanakamfumu hajafahamishwa kupitia hizo njia mbili, kwa hiyo adhabu yake haijaanza mpaka sasa hivi na hiyo inatoa ruhusa kwake kuendelea na kazi zake za ukocha na kusimamia academy yake au kazi zozote za mpira kwa sababu TFF haijakidhi hayo matakwa ya kisheria.”

“Nimesoma maelezo ya hukumu ambayo nimeyapata kwenye internrt ambayo sio rasmi nimegundua kwamba kuna sababu tano nzito ambazo nimezibaini za kukatia rufaa.”

Haji Manara amezungumzia mechi yao na Al Masry

$
0
0

Leo Jumamosi Machi 3, 2018 afisa habari wa Simba Aji Manara amekutana na waandishi wa habari kuzungumzia mambo mbalimbali yanayohusu mchezo wao wa Caf Confederation Cup dhidi ya Al Masry unaotarajiwa kuchezwa siku ya Jumatano Machi 7, 2018.

Miongoni mwa mambo ambayo manara amezungumzia ni viingilio, waamuzi, pamoja na maandalizi ya Simba kuelekea mchezo huo.

Mechi hiyo itachezwa kuanzia saa 12:00 jioni kwenye uwanja wa taifa, Manara amesema wamepanga muda huo kwa sababu mechi itachezwa siku ya kazi hivyo muda huo utakuwa rafiki kwa wadau wote.

“Tumeweka viingilio vya aina tatu, mzunguko pamoja na Orange kiingilio itakuwa ni Tsh. 5000, VIP B Tsh. 15,000 na VIP A Tsh. 20,000.”

“Kuanzia keshokutwa vituo vyote vya Puma na sehemu nyingine zote ambazo nitazitaja kesho zitauzwa tiketi na watu wa Selcom kama ilivyo dasturi. Tutajitahidi kuwe na centre nyingi ili watu wapate tiketi kwa urahisi.”

“Klabu ya Al Masry itawasili kesho (Jumapili) jioni saa 12, siku ya Jumatatu jioni wafanya mazoezi kwenye uwanja wa taifa kama kanuni zinavyotaka kwa sababu Jumanne kutakuwa na mchezo wa klabu bingwa kati ya Yanga dhidi ya Township Rollers.”

“Waamuzi watawasili siku ya Jumatatu saa 10 jioni kutoka Afrika Kusini lakini mechi kamishna anatoka Elitrea ambaye atawasili siku moja pamoja na waamuzi.”

“Pre-match meeting itafanyika siku ya Jumanne jioni kwenye hotel ya Golden Tulip.”

“Maandalizi mengine ndani ya timu yetu yanakwenda vizuri, timu imeingia kambini leo baada ya mchezo wa jana wa ligi kuu.”

Azam wamefafanua basi lao kuwapokea waarabu wa Simba

$
0
0

Kama umeshuhudia picha zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii, wapinzani wa Simba kwenye michuano ya kombe la Afrika, timu ya Al Masry wameonekana wakitumia basi la Azam kutoka uwanja wa ndege wa Mwl JK Nyrere kuelekea hoteli ambayo wamefikia.

Jambo hilo limezua maswali mengi na mijadala mbalimbali huku wapo pia waliohoji iweje klabu ya Azam iwapatie usafiri wapinzani wa Simba?

Jafar Idd amefafanua kuhusu basi lao kutumika kuwabeba Al Masry kuelekea mchezo wa Caf Confederation Cup dhidi ya Simba.

“Azam FC tuna biashara nyingi ambazo tunafanya, tunamiundombinu mingi pia. Kama ilivyo kwa uwanja wa Azam Complex, ambapo mtu anaweza kuomba kuutumia baada ya kufuata taratibu zinazotakiwa ikiwa ni kuandika barua kwa CEO.”

“Baada ya barua kutufikia tutaangalia ratiba ipoje kama inaruhusu basi tutaruhusu uwanja kutumiwa lakini muhimu ni kufuata taratibu.”

“Basi la Azam sio mara ya kwanza kutumika kubeba timu za nje. Zimekuja timu mbalimbali na kutumia basi la Azam lakini pia timu za taifa zinapokuja kucheza na timu yetu ya taifa basi letu hutumika.”

“Kwa hiyo Simba walituandikia barua ya kutaka kutumia basi letu ili kuwapokea wageni wetu.”

Simba na Al Masry zitacheza mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya kombe la shirikisho Afrika siku ya Jumatano Machi 7, 2018 uwanja wa taifa kuanzia saa 12:00 jioni.


Shaffih Dauda baada ya Yanga kupoteza mechi ya kimataifa nyumbani

$
0
0

Kumekuwa na maoni mengi na mitazamo tofauti baada ya mechi ya Caf Champions League kati ya Yanga dhidi ya Township Rollers mchezo ambao umeshuhudia yanga ikipoteza nyumbani kwenye uwanja wa taifa kwa kufungwa 2-0 ikiwa ni mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza.

Wengi wao wametoa maoni kwa kuangalia matokeo ya uwanjani kwa upande wa Shaffih Dauda pia ametoa maoni yake kwa kueleza sababu kadhaa za Yanga kupoteza mechi hiyo lakini amegusia mambo mengi ikiwemo ubora wa ligi, maandalizi pamoja na vitu vingine

Wakati mwingine matokeo kama haya yanatupa mtazamo mpana wa kuangalia mambo mengine ambayo sisi tunayafanya na kuridhika nayo kutokana na mazingira ya kwetu na tunaona tupo sawa labda kutokana na mazoea.

Kwenye mechi kama hizi ili uweze kufanya vyema, ni lazima yawepo maandalizi yanayotokana na mamo mengi, kuna maandalizi ya makocha na benchi la ufundi kufanya kazi yao ya kumtambua mpinzani wanaekutana naye, hilo ni jambo la kwanza lakini wawe wanapata support kutokana na mfumo wa ligi yao na nchi yao kwa ujumla.

Yaani mpango wa maendeleo ya mpira kitaifa katika nchi yao, mamlaka husika wametekeleza majukumu yao kwa kiasi gani? Ukija kwenye ligi yao ‘Botswana’ inaendeshwa kwa utaratibu upi? Level ya ushindani kwenye ligi yao ipoje? Performance na viwango vya wachezaji kutoka katika timu tofautitofauti upoje?

Vitu vyote hivyo ni matokeo ya wadau wengi kwa maana ya vilabu vyenyewe vinamajukumu yake kuhakikisha wanaandaa mifumo mizurikutengeneza klabu zao, mamlaka zingine kwa mfano zinazosimamia ligi jukumu lao ni kuhakikisha ligi inakuwa ya ushindani ambayo itatoa bingwa ambaye atakwenda kushindana na mabingwa kutoka kwenye mataifa mengine na akawawakilishe vyema kuonesha ni namna gani ligi yao ilivyo bora na kwenda kuitangaza. Sasa kwetu, vitu vyote hivyo huwa hatuvipi kipaumbele huwa ‘tunajifanyiafanyia’.

Kilichobadilisha matokeo kwenye mechi ya Yanga na Township Rollers ni level ya performance, wenzetu level yao ilikuwa juu ukilingabisha na performance ya Yanga, Yanga walikuwa kama asilimia 50 ukilinganisha na wale Township Rollers kuanzia mchezaji mmojammoja kuja kwenye timu nzima. Naona baadhi ya watu wanazungumzia mchezaji mmojammoja kama vile Kessy, Tshishimbi, Chirwa, Yondani, lakini timu ndiyo inakupa matokeo.

Kwa mfano Kessy anafahamika kwa style yake ya uchezaji, ni ‘wing back’ anayekimbia pembeni, lakini ili upate kilicho bora kutoka kwake lazima apate ‘connection’ ya wenzake ambao wapo maeneo mengine watekeleze majukumu yao ili yeye anapokimbia na kupiga pasi ndani na anapokimbia kwenye mstari wa pembeni akutane na mpira kwenye nafasi aweze kupiga pasi ya mwisho wakati huo mshambuliaji awe amefika eneo la kufunga.

Wale Township Rollers kuanzia kwenye eneo lao la ulinzi walikuwa bora na walikuwa wanajua nawafanya kitu gani na ili waweze kutekeleza mipango aliyoizungumzia mwalimu, jambo la kwanza ni lazima wawe fit. Level ya fitness ya wachezaji wa Yanga unaweza kuiona iko chini ukilinganisha na wachezaji wa Rollers hata ukiangalia walivyokuwa wakigombea mipira ‘one against one’ walikuwa wanafanikiwa zaidi kuliko wachezaji wa Yanga. Walipokuwa wana mpira kwenye himaya zao hakuna mchezaji wa Yanga aliyekuwana uwezo wa kuuchukua.

Ukiangalia goli la pili, issue sio pasi kwa sababu unaweza ukapiga pasi hata 100 lakini upo kwenye eneo lako ambalo halimpi presha mpinzani ‘less pressure area’ mpinzani wako atakuwa anakuangalia tu unavyojifurahisha lakini unapovuka kwenda kwenye eneo la mpinzani ukiwa uanaendelea kupiga pasi maana yake wapinzani watatakiwa kuwa fit kwa kiasi kikubwa kwa sababu watatakiwa kukimbia sana kuziba ma-gape na kukaba ili kuuchukua mpira na nyinyi mcheze kwenda kwao.

“Simba inauwezo wa kuifunga Al Masry magoli 4 lakini kazi lazima ifanyike”-Shaffih Dauda

$
0
0

Wawakilishi wa Tanzania kwenye kombe la shirikisho barani Afrika (Caf Confederation Cup) wekundu wa Msimbazi Simba, wanatarajia kushuka uwanjani leo jumatano februari 7, 2018 kucheza dhidi ya Al Masry kutoka misri.

Kuelekea mchezo huo, Shaffih Dauda ambaye ni mchambuzi wa michezo kutoka Clouds Media Group anaamini Simba inauwezo wa kupata matokeo kwenye uwanja wa nyumbani lakini inabidi kazi ya ziada ifanyike na wasitarajie mchezo utakuwa kama mechi za ligi yetu ya Tanzania bara. Dauda pia ameonesha hofu yake kwa safu ya ulinzi ya Simba ambayo ameitaja kuwa inafanya makosa mengi, kwa hiyo amesema kama eneo la ulinzi la Simba litakosa umakini huenda Al Masry wakamaliza biashara uwanja wa taifa.

Unapataje matokeo baada ya mechi mbili? Kufuzu kwenda hatua inayofuata sio matokeo ya mechi moja, Simba wenyewe wanajua wanamechi mbili Al Masry pia wana mechi mbili.

Kila upande una namna ambavyo unaangalia hiyo mechi ya kwanza wanaingiaje, Al Masry na tabia ya timu za Afrika ya Kaskazini, mechi ya kwanza kama inakuwa ya ugenini kuna aina ya mechi huwa wanawaacha nyumbani baadhi ya wachezaji wao wa kutegemewa kabisa. Wanachukuwa wachezaji wengine ambao wanakuja kutekeleza plan ya kucheza hiyo mechi ya ugenini ambapo mara nyingi huwa wanajilinda sana na kutokubali kupoteza mchezo.

Lengo lao mama huwa kutoruhusu kufungwa goli, lakini inapotokea wakapoteza basi isiwe kiasi kwamba mechi ya pili itakuwa mzigo. Kwa hiyo changamoto ya kwanza ambayo Simba wanayo ni kuhakikisha wanawafungua Al Masry ili kuhakikisha malengo yao ambayo sihitaji kuwa karibu na kocha Lechantre na benchi la ufundi lakini mipango yao ni kuifunga Al Masry kwa tofauti ya magoli mengi ili wawe na akiba nzuri ya magoli.

Wanapokwenda ugenini waende na plan ya kuwachanganya wapinzani wao huku wakipoteza muda dakika 180 zikamilike halafu mwenye matokeo mazuri ya mechi zote mbili afuzu kwenda hatua inayofuata.

Al Masry chini ya kocha wao Hosam Hassani tusitemee wataishambulia Simba kama nyuki lakini watakuwa makini kutumia mapungufu ya Simba kupata faida. Moja ya changamoto kubwa kwetu ni kukosa umakini, wenzetu wana umakini wa hali ya juu sana, hawafanyi makosa ya ‘kipumbavu’ mara kwa mara kwa hiyo ili uweze kufanikiwa jambo lako inakuidi ufanye kazi kubwa ili wafanye makosa halafu utumie makosa hayo.

Tusitarajie kuona yale magoli mepesi ya 4G ambayo wanafunga akina John Bocco na Okwi kwenye ligi yetu, Simba inauwezo wa kufunga magoli manne lakini kazi lazima ifanyike kwa umakini wa hali ya juu mno.

Simba wako vizuri sana kwenye safu ya ushambuliaji lakini wanafanya makosa mengi sana kwenye eneo lao la ulinzi ndiyo maana nadiriki kusema, Al Masry wanaweza kuwa wamekuja kwa lengo la kujilinda lakini kwa makosa yanayofanywa kwenye eneo la ulinzi la Simba wanaweza wakafunga magoli na kuimaliza shughuli hapahapa.

Al Masry wamekuja na kufikia kwenye hoteli yenye hadhi kubwa Dar es Salaam wako vizuri, hawajaja wamepakatana kwenye  Coaster  wamekunja miguu hadi imevimba kama timu zetu za mikoni ambazo hazina hata uhakika wa kula vizuri wala hawajui watarudije walikotoka. Hawa wamekuja kazini kwa hiyo sio mechi nyepesi, ni mechi ngumu lazima Simba walitambue hilo na wafanye kazi.

Mashabiki wajitahidi kuheshimu matokeo ya uwanjani, kwa mfano baada ya Yanga  kufungwa na Township Rollers kuna mashabiki wametukana na kulaumu baadhi ya wachezaji, ikitokea timu yako imepoteza kubali matokeo huzunika lakini si kwa kulaumu wachezaji wala benchi la ufundi kwa sababu ndiyo haohao wakishinda tunawashangilia.

Ndondo Cup 2018 ‘washtue wana!’

$
0
0

Msimu wa Ndondo Cup 2018 umezinduliwa rasmi leo Machi 9, 2018 Dar es Salaam na kamati ya mashindano hayo chini ya mwenyekiti wake Shaffih Dauda. Uzinduzi huo umefanyika katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Escape One na kutangaza rasmi timu za Dar kuanza kujisajili rasmi katika ofisi za chama cha soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kwa ada ya shilingi 300,000.

Kama ilivyo ada ya mashindano hayo baada ya Dar es Salaam yataelekea katika mikoa ya Mwanza pamoja na Ruvuma, ambapo kwa Ruvuma itakuwa ni mara ya kwanza wakati mwanza ikiwa ni mara ya pili.

Shaffih Dauda ambaye ni mwenyekiti wa mashindano hayo amefafanua zaidi baadhi ya mambo kupitia video ambayo unaweza kuangalia hapa chini kwa kubofya ‘play’.

Wakili ameeleza kesi ya Wambura ilivyoendeshwa

$
0
0

Kamati ya maadili ya TFF imetangaza kumfungia imemfungia kutojihusisha na masuala ya soka kwa kipindi chote cha maisha yake Makamu wa RAIS wa TFF Michael Wambura baada ya kumtia hatiani katika makosa matatu tofauti ambayo alikuwa akituhumiwa nayo.

Wakaili wa Wambura Emanuel Muga ameeleza namna kesi ya mteja wake ilivyoendeshwa na kamati ya maadili ya TFF kabla ya kufikia hukumu ya kumfungia maisha kujihusisha na masuala ya soka. Muga amesema kesi hiyo haikufuata kanuni na sheria za maadili.

“Kamati ilikuja kufanya maamuzi lakini haikuwa tayari kumsikiliza mtu wala kupokea ushahidi wa aina yoyote. Ile kamati ya maadili ililetewa mashtaka na secretariat, secretariat wakati inaletewa mashtaka haijatuonesha maazimio ya kamati tendaji yaliyoazimia kwamba suala la Michael Wambura linapelekwa kwenye kamati ya maadili hayo ndio maamuzi ambayo yanapaswa kufanywa na TFF.

“Huo muhtasari haukuoneshwa na haukuwepo kwenye karatasi zote zilizokuwepo kwa hiyo ni kundi tu lilikutana likafanya maamuzi lakini hakukuwa na msingi wa kamati tendaji hilo ni jambo la kwanza, la pili ni namna walivyopeleka wito hakukuwa na utashi wa kutoa nafasi ya kusikilizwa kwa yule ambaye alikuwa anashtakiwa.

“Kanuni za maadili zinasema kwamba, ukishapokea wito una siku tatu za kuitikia kwa kufika pale unapoitwa ili utoe maelezo yako lakini wakati tupo kwenye kamati ya maadili, mwanasheria wa TFF alisema kwamba waliandika wito Machi 13, huo wito wakaupeleka kwa wambura usiku wa siku hiyohiyo ili aje Machi 14, 2018.

“Wambura hakuwepo nyumbani kwake hiyo Machi 13 lakini pia kupeleka wito nyumbani kwa mtu sio utaratibu wa kisheria kwa hiyo haukupokelewa kwa sababu hakuwepo.

“Nikapewa maelekezo kama wakili niende kwenye hicho kikao, lakini ukifika kwenye kikao kama hiki unachofanya ni kuhakikisha ule mchakato unakuwa wa kisheria ili maamuzi yatakayotoka yawe ni maamuzi yaliyozingatia sheria.

“Jambo la kwanza nililowaonesha wanakamati lilikuwa linahusiana na kanuni kwamba wito uliandikwa Machi 13 kanuni inasema angalau tuna siku tatu kuja kuitikia kwa hiyo hizo siku tatu vipi? Nikaambiwa hilo suala la kisheria tutalitolea uamuzi na uamuzi utatoka baada ya wao kujadiliana. Nikatolewa nje kwa muda mfupi wakajadiliana kisha nikarudishwa nikaambiwa hilo wamelikataa niendelee kumtetea mteja wangu.

“Baada ya hilo nikawaelekeza kwenye kanuni nyingine ya maadili inayosema, ukishapokea wito baada ya siku tatu unaenda mbele ya kamati lakini sio mnaanza kesi, unaileza kamati kwamba utakuwa na mashahidi kadhaa, utapeleka vielelezo kadhaa kwa hiyo mpange muda wa kusikilizwa.

“Kamati ikishajua  hivyo ikaridhika kila mtu ameshajiandaa, inatoa muda wa kusikilizwa, hayo ni matakwa ya kisheria kwenye kanuni. Nikawaambia naomba tufuate sheria, mwenyekiti wa kamati akasema nisiwapotezee muda bila hata kuiangalia hiyo sheria badala yake nikaambiwa napoteza muda nachotakiwa kusema ni kafanya au hajafanya.

“Nikamwambia mwenyekiti sio utaratibu wa kisheria na hakuna kesi inayoendeshwa kwa siku moja duniani kote, hata CAS wanatoa siku 21 lakini wao walikuwa wanataka siku moja wamalize jambo waondoke zao.

“Baada ya mvutano wakasema ngoja tutoe maamuzi, nikatoka nje nilivyorudi wakatoa maamuzi wakasema tumetoa maamuzi kesho tutatoa hukumu. Tulikuwa tunabishania suala la kisheria badala ya kutoa maamuzi kwamba watafuata sheria au la wakasema kesho tutatoa hukumu.

“Nikauliza hiyo hukumu itakuwa ya kujaribu kufafanua kama mtafuata sheria au hukumu ya kesi ya msingi? Wakasema hukumu ya kesi ya msingi, nilishangazwa!”

Baada ya kufungiwa, Wambura aibua mapya TFF

$
0
0

Ukimwaga mboga, namwaga ugali ni miongoni mwa misemo maarufu ya lugha ya Kiswahili ambao unaweza kutimia baada ya Makamu wa Rais wa TFF kufungiwa maisha kujihusisha na masuala ya soka kufuatia kutiwa hatiani na kamati ya maadili ya TFF.

Baada ya hukumu kutangazwa, Michael Wambura alizungumza na vyombo vya habari akitoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo lakini amesema kufungiwa kwake ni kwa hila na njama iliyopangwa na watu wachache.

Wambura ameibua hoja kadhaa akiituhumu TFF kuajiri baadhi ya watu bila nafasi hizo kutangazwa kama taratibu na kanuni zinavyoelekea, lakini pia ameituhumu tff kutumia kiasi kikubwa cha pesa kwa muda mfupili lakini hakuna kinachoonekana kufanywa kulingana na kiasi hicho cha pesa.

“Ni kweli kulikuwa na kikao lakini bado nasisitiza kilikuwa cha hila kilikuwa ni kikao ambacho kimeandaliwa kwa ajili ya kutoa maamuzi bila kujali hoja ambazo zitakwenda kujadiliwa. Ninasema hivyo kwa sababu siku ya Jumatatu nilikuwa TFF niliongea na Rais wa TFF pamoja na Katibu, Jumanne niliongea na Rais wa TFF lakini wote hawakuniambia kama kuna jambo lipo TFF linanihusu mpaka Jumanne nasafiri hakuna chochote kutoka TFF kuja kwangu lakini jioni saa 12 wanakwenda nyumbani kwangu kupeleka mashtaka.

“Kwa hiyo tayari kuna hila ambazo nilikuwa nimeziona katika jambo hilo, katika mashtaka yao msingi mkuu umeegemea katika kufoji document hakuna anaebisha walikuwa hawadaiwi, wote wanakiri kudaiwa katika barua mbalimbali za TFF lakini wanasema kwamba document zimefojiwa.

“Kiutaratibu kuna njia mbili, njia moja ni kupeleka polisi wakaangalie kama document imefojiwa baada ya kupata majibu ya polisi mnaelekea katika mkondo washeria ndio msingi wa hizi kamati. Hizi kamati haziwezi kuingia mahali ambapo kosa ni la jinai, ufojaji ni kosa la jinai sio la kimaadili kwa hiyo ilipaswa iende katika mfumo wa sheria ya jinai sio mfumo wa kimaadili.

“Kampuni ambayo wanasema document yake imefojiwa ilipaswa iitwe kwa sababu kampuni inaishi na ina wakurugenzi, kwa hiyo wakurugenzi ndio walipaswa kuitwa ikishajulikana hivyo kinachofuata ni kupelekwa polisi na kushtakiwa kama mhalifu mwingine lakini kwa sababu wameona hawana kesi ya msingi wakaamua kukaa na kamati walizoziunda wenyewe ili wamtoe Wambura katika nafasi kitu ambacho hakikubaliki.

“Kwa hiyo ninachoona yote haya ni kutokana na matatizo yaliyopo ndani ya TFF, jambo la miaka 14 iliyopita unataka kulijadili kwa siku moja kwa kumpa mtu notice usiku asubuhi aje mbele ya kamati, viongozi walikuwepo wengi wamepita hapo katikati wote walitakiwa waje kutoa ushahidi lakini hawakuitwa? Kwa nini walilipa? Au aliyelipwa alivunja ofisi?

“Isije ikawa kuna mtu amejilipa ndani ya TFF kwa jina la ile kampuni na kitu ambacho kipo, kuna watu wamelipwa pesa kwa kutumia jina la hiyo kampuni wakati hizo pesa hazijalipwa kwa kampuni ndiyo maana wanashindwa kutoa hizo document ndiyo maana tunasema walete nyaraka za hayo malipo kama hawajaiba wao wenyewe wanashindwa.

“Kama wanasema nimefoji barua nipo tayari twende polisi na mahakamani ndio maana nasema hili jambo limetengenezwa kimkakati halina mashiko hata kidogo ya kisheria, halina ushahidi ni jambo la uongo na kizandiki limetengenezwa na kikundi cha watu ambao wanaamini nikitoka kama mwenyekiti wa fedha mambo yao yatakuwa mazuri.

“Mimi nimechaguliwa na mkutano mkuu kwa zaidi ya kura asilimia 80, siwezi kuondolewa na watu watatu ambao hawakuchaguliwa hawana dhamana ya mkutano mkuu, haiwezekani. Kama unadhani nina kosa kanishtaki kule.

“Ni kweli kwamba kila uongozi unapokuja unakuwa na taratibu zake , sisi taratibu zetu za kiutendaji ni kwamba, nafasi ya katibu mkuu wa TFF lazima itangazwe kama makatibu wakuu wengine walivyopita, nafasi inatangzwa watanzania wenye sifa wanaomba kupitia makampuni ambayo ni huru, wanafanya usaili wanaajiriwa.

“Sisi pale kwetu kuna shida kidogo kuna watu wengine bado wana kazi mbili, kuna mtu mwinngine ameajiriwa huku anakuja pale kama secondment wakati kuna watanzania wengi wanaweza kuomba na kuajiriwa, sasa mtu ana kazi mbili.

“Suala la katibu mkuu anapaswa kuajiriwa, tulipochaguliwa kaimu katibu mkuu alikuwa Salum Madadi kwa sababu madadi alikuwa majiriwa wa TFF kwa hiyo alikuwa anakaimu nafasi kwa sababu alikuwa mwajiriwa wa TFF baadaye tulipokuja kumpa nafasi Wilfred Kidao yalikuwa ni makosa kwa sababu sheria zinakataza mjumbe wa mkutano mkuu kuajiriwa TFF na kidao ni mwenyekiti wa TAFCA hawezi kuajiriwa akawa mjumbe wa mkutano mkuu wakati huohuo.

“Tuna matatizo mengi, TRA wanatudai lakini bado tunakusanya kodi na tunazitumia, tunamatatizo ya fedha za wafadhili tunazihamisha matokeo yake ligi ya wanawake inasimama, wakati mwingine hata ligi kuu inasimama kwa sababu hakuna pesa lakini Azam wamelipa kwa hiyo tuna shida.

“Tunaposema tunataka tuweke nyumba kwenye mstari masuala ya kodi yaeleweke kodi zinazopokelewa na bodi zikalipwe TRA badala ya kuletwa TFF ndio mgogoro unapotokea. Bodi ya ligi ina kusanya kodi toka Azam, na wadhamini mbalimbali lakini kodi zile zinakuja kwetu TFF zikishakuja na kutumika mwenyekiti wa kamati ya fedha akisema hapana sio sahihi inakuwa issue.

“Matatizo mengi tutakuja kuyaona siku chache zijazo, watanzania watanielewa kwamba ndani ya TFF kuna matatizo makubwa sana na sio madogo kama watu wanavyofikiria, siku chache zijazo tutakuja kuyazungumza.

“Tumeshatumia kiasi cha shilingi 3 bilioni ndani ya miezi nane, kuna nini tumefanya? Zinapita tu. Jambo moja linapoanza uzuri wake linafuata na jingine kwa hiyo tutakwenda mpaka mahali tutakuwa sawa na ninaamini watafuata ninachokisema, bado tunahitaji kusafisha TFF kwa sababu haiko sawa.”

Wambura ana haki ya kukata rufaa?

$
0
0

Mwenyekiti wa kamati ya maadili hamidu amesema baada ya hukumu ya kumfungia maisha Makamu wa Rais wa TFF Michael Richard Wambura kutojihusisha na  shughuli za soka, Wambura ana nafasi ya kukata rufaa kwenye kamati ya rufaa na kusikilizwa.

“Nafasi ya kukata rufaa anayo na kamati ya rufaa ipo, kama atakwenda pale anakaribishwa”-Hamidu Mbwezeleni, mwenyekiti kamati ya maadili.

Kwa mujibu wa wakili wa Wambura Bw. Emanuel Muga amesema, mchakato wa shauri la mteja wake haukufuata kanuni wala sheria kufikia hukumu iliyotolewa na kamati ya maadili.

Tuhuma tatu ambazo zilikuwa zinamkabili Wambura ni kupokea ama kuchukua fedha za shirikisho (TFF) za malipo ambayo hayakuwa halali ikiwa ni kinyume na kanuni za maadili ya TFF, kughushi barua ya kuelekeza alipwe malipo ya kampuni ya Jet System Limited huku akijua malipo hayo siyo halali, shitaka la tatu ilkuwa ni kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya shirikisho.

Mwanasheria alivyochambua hukumu ya makamu wa Rais TFF

$
0
0

Baada ya kamati ya maadili kumfungia makamu wa rais wa TFF Michael Richard Wambura kumekuwa na mijadala mingi miongoni mwa wadau wa soka, baadhi wakihoji kama kanuni na sheria zilifuatwa kulingana na namsha shauri linalomhusu Wambura lilivyoendeshwa kwa haraka na kutolewa hukumu.

Kwa mujibu wa tff, Machi 13 2018 Wambura alipewa wito ili afike mbele ya kamati ya maadili machi 14, 2018 kwa ajili ya kutoa maelezo juu ya tuhuma tatu zilizokuwa zinamkabili, machi 15 tff ikatangaza hukumu ya kumfungia maisha Wambura kujihusisha na shughuli za soka.

Baadhi ya wanasheria wametoa mtazamo wao juu ya kinachoendelea juu ya sakata hilo, Alex Mgongolwa ni mmoja wa mawakili waandamizi nchini ametoa ufafanuzi juu ya suala zima la kamati ya maadili inavyotakiwa kufanya.

“Kuna kuwa na kamati ya maadili lakini kuna kuwa na kamati ya rufaa ya maadili ili kumpa nafasi mtu ambaye hajaridhika na maamuzi ya kamati ya maadili kuweza kukata rufaa kwenda kamati nyingine. Ni mfumo tu wa utoaji haki ndio ulikuwa unatuongoza katika kutengeneza kanuni hizi, dhamira ya kamati ya maadili, kamati ya nidhamu ni mfumo unaoitwa nusu ya mfumo wa mahakama.

“Mfumo wa nusu ya mahakama ni ambao unatoa haki na unafuata kanuni za msingi za utoaji haki kwa mfano haki ya kusikilizwa, kutoa ushahidi, na ushahidi wenyewe kufanyiwa upembuzi na kufikia uamuzi. Kwa hiyo kwa maana ya kamati, dhamira ni yake ni kutoa haki lakini kwa maana ya utendaji na utekelezaji inadhamiriwa pia kamati hizo zitende haki.

“Makosa yanayopelekwa kwenye maadili ni vizuri ikafahamika si kila kosa ni la maadili, lazima utofautishe makosa ambayo ni ya kimaadili kwa maana yale yanayowabana viongozi wawe katika tabia ambayo haiudhalilishi mpira hayo ndiyo maadili ambayo yameainishwa katika kanuni. Kama kiongozi ukikiuka maadili hayo unapelekwa kwenye kamati ya maadili. Kama kosa ni la kinidhamu unapelekwa kwenye kamati ya nidhamu kama kosa linahusiana na sheria za nchi (linahusiana na mambo ya jinai) unapelekwa katika sheria za mfumo wa nchi.

“Ni vizuri ikafahamika miundo hiyo ipo hapo kwa ajili ya kutenganisha mamlaka na madaraka.

Namna kesi ya kumfungia Michael Richard Wambura ilivyoeneshwa kwa jinsi ulivyofuatilia unafikiri taribu na kanuni zilifuatwa?

“Kwa kuwa jambo hilo bado lina nafasi ya kwenda kwenye kamati ya rufaa, nisingependa kulizungumzia sana lakini ambacho ningetaka nizungumze kwa wakati huu lililopo ni kwamba kanuni za msingi za uendeshaji mashauri ya kutoa haki ni lazima zifuatwe na tunavyosikia ni kwamba kanuni hizo zilifuatwa. Kwa hiyo kwa yeyote yule ambaye hajaridhika na uamuzi huo ndio maana kanuni hizo zimetoa nafasi ya kwenda kwenye rufaa na hata rufaa hiyo ukiwa hujaridhika na maamuzi bado mfumo wa utoaji wa haki wa mpira wa miguu unatoa nafasi kubwa zaidi kwenda ngazi nyingine mpaka Caf.

“Kwa maana ya kukosea, mimi kama mwanasheria chombo kukosea katika utoaji wa maamuzi ni kitu ambacho nakitazamia, ni cha kawaida na ndiyo maana kunakuwa na ngazi mbalimbali za kukata rufaa na chombo kile kinachosikiliza rufaa kinajikita katika kuona kanuni za utoaji haki zilifuatwa? Huwezi ukalijua hilo mpaka mlalamikaji akueleze kwamba anachokilalamikia ni nini?


Hukumu ya Wambura pasua kichwa

$
0
0

Mhadhilizi wa sheria chuo kii cha Tumaini Dar es Salaam Edwin Mgandila ametoa maoni yake juu ya utaratibu uliotumika kusikiliza shitaka la wambura na utaratibu upi unaotakiwa utumike

“Ni wazi kwamba kamati ya maadili ya TFF ina mamlaka ya kisheria na kimahakama,  kukiwa na organ yenye mamlaka ya kimahakama wakati wa kutenda haki inaongozwa na misingi ya kisheria kwa mfano msingi mmoja wapo ni wa kikatiba kwamba mtu anavyohukumiwa kuna mchakato wa kisheria ambao haukwepeki. Kama hiyo mamlaka ya maamuzi imetoa maamuzi ni lazima impe sababu za maamuzi yale hiyo ndio misingi ya kisheria.

“Inapokuwa imetokea hivyo kama kuna hatua za kukata rufaa na kuna vyombo vya kusikiliza rufaa vinaweza vikasikiliza rufaa  kama hakuna mchakato huo wa rufaa, wanaweza kwenda mahakamani kwa sababu kitu nachoweza kuwashauri TFF ni kurudia upya mchakato wa haki ya bwana Wambura na kufuata utaratibu wa kisheria siku zote kwa sababu hiyo hukumu ilikuwa ‘tainted na irregularity’ na hukumu ikiwa hivyo (‘tainted na irregularity’) ina madhara yake inapokuja suala la rufaa, inaweza ikaamriwa kufanya maamuzi upya kwa kuzingatia taratibu za kisheria au mahakama ya juu inaweza ikatengua yale maamuzi ya awali na kumtangaza yule mtu hana hatia au ameonewa.

“Sheria inasema kwamba, sio haki itendeke tu bali ni lazima bali ni lazima haki ionekane ikitendeka. Nimeufuatilia vizuri mchakato wa bwana wambura na kitu kingine nilichokifahamu ni tuhuma za kufoji unapozungumzia kufoji nyaraka hiyo ni miaka saba hadi 14 jela maana yake ni kosa la jinai, inapokuwa kosa la jinai ukiangalia shria ya ushahidi ya Tanzania inakwambia kwamba, yule anayekutuhumu ni lazima athibitishe.

“Kiwango cha kuthibitisha ni pasipo na shaka yoyote kwa hiyo pale walitakiwa wathibitishe pasipo shaka yoyote na kuthibitisha pasipo shaka yoyote sio jambo rahisi na watafanya hivyo iwapo mchakato mzima wa kisheria ulifuatwa, hiyo ndio position ya kisheria.

Kumekuwa na mkanganyiko kidogo, kamati ya maadili inaweza kujiridhisha kwamba kuhusu nyaraka kughushiwa au ilitakiwa ipeleke kwenye mamlaka nyingine yenye uwezo wa kuthibitisha halafu irudishe majibu kwenye kamati ya maadili?

“Ile kamati haina uwezo wa kuthibitidha hilo, kuna vitengo maalum vya polisi na kuna watu tunawaida mashahidi wa kiutaalam, inatakiwa atafutwe mtaalam kwa sababu jambo la kughushi ni kosa la jinai na mamlaka yenye uwezo wa kufanya uchunguzi wa kosa lolote la jinai ni polisi kwa hiyo suala ambalo lilitakiwa kupelekwa kwenye mamlaka husika.

Rufaa ya Wambura imesheheni sababu 5

$
0
0

Wakili anaemtetea Michael Wambura, Emanuel Muga amesema kwamba, wao wameamua kukata rufaa ili kutafuta haki ya mteja wake.

Muga amesema katika rufaa hiyo imesheheni masuala ya kisheria na kuna sababu tano za msingi zilizowafanya waamue kupeleka rufaa mbele ya kamati ya maadili ya rufaa.

“Kinachofuata ni hatua ya rufaa, tumeshaandaa rufaa na ipo tayari tumeshailipia kwa mujibu wa kanuni lazima ilipiwe silingi milioni moja (1,000,000) na tumeanza utaratibu wa kuisajili pale TFF ndani ya siku tatu ambazo zimetolewa.

“Rufaa imesheheni masuala ya kisheria, ina sababu tano za msingi na tutakuwa tayari kwenda mbele ya kamati ya rufaa ya maadili ili tuweze kuzifafanua hizo sababu tano.

Hukumu kutoka kamati ya maadili mmeshaipata?

“Hukumu tumeipata ikiwa imechapwa lakini kwenye tovuti na tuliisikiliza lakini kanuni hazisemi kwamba tuiambatanishe wakati kunakata rufaa kwa hiyo tumeamua kukata rufaa ingawa haijatufikia rasmi kwa sababu tumekata rufaa kwa hati ya dhalura kwamba kamati ya rufaa ya maadili iitwe haraka kwa hati ya dharura ili isikilize hili suala itolee maamuzi ili mambo mengine yaendelee.

“Wambura hawei akabaki amefungiwa tu ni mtu ambaye anamajukumu mengi ya kitaifa na kimataifa, ikumbukwe kwamba aliteuliwa kuwa mechi kamishna wa mechi itakayochezwa mwezi ujao ya U20 kati ya Kenya na Rwanda kwa hiyo hatima yake lazima ijulikane kabla ya mwezi Aprili ili aweze kufanya hayo majukumu.

“Kwa hiyo tunaiomba TFF kwa hati ya dharura iitwe hiyo kamati ya rufaa ya maadili ili iweze kusikiliza na hatma ijulikane.

Mkurugezi kampuni iliyokuwa inaidai TFF yupo tayari kutoa ushahidi kesi ya Wambura

$
0
0

Mmoja wa wakurugenzi wa Jeksc Systems Limited iliyokuwa inaidai TFF Jost Rwegasira ameibuka na kuzungumzia kuhusu barua au nyaraka za kampuni hiyo zinazodaiwa zilighushiwa.

Rwegasira amesema yupo tayari kutoa ushahidi wake mahali popote endapo utaratibu wa yeye kufanya hivyo utafuatwa lakini kwa sababu tayari hukumu imeshatolewa hawezi kuweka jambo hilo hadharani labda ikitokea ameitwa mamlaka itakayokuwa ikisikiliza rufaa ya kesi hiyo.

“Uamuzi wa mahakama ya maadili umeshatoka, wametoa uamuzi bila kuuliza Jeksc. Nimefuatilia kila kitu tangu kilivyotangazwa lakini sina uwezo wa kuingilia mambo ya TFF lakini kwa kuwa uamuzi umeshatoka, kwa hiyo nilichonacho ni ushahidi kwa atakaekata rufaa au yule atakaekuwa anasikiliza rufaa.

“Naomba umma unielewe, wakati uamuzi umeshatolewa inamaana upande mmoja una uhakika na unachosema na upande wa pili unaopinga una uhakika kwa unachosema kwa hiyo mtu wa tatu atakaepelekewa rufaa kama itakuwepo ndiye mwenye mamlaka ya kumuomba mlalamikaji au mlalamikiwa kupeleka ushahidi.

“Naweza kutoa ushahidi kwa sharti moja, ni ipi barua inayolalamikiwa kwamba ni ya kufoji? Mimi sijaipata, siwezi kukaa pembeni nikatoa ushahidi kwamba hiyo barua sio ya kufoji mpaka wewe mwenye maswali uwe nayo uniulize barua hii unaijua?

“Jambo la pili kwa sababu unapinga hukumu ambayo ilishaotolewa, lazima uwe na ushahidi ambao umeombwa kutoa kwamba hii barua iliyoletwa kwenye kesi sisi tumeiona ni feki lakini kama sijaiona hiyo barua nina kubali nini au nakataa nini?

Shauri likienda mbele kwenye kamati ya maadili ya rufaa upo tayari kutoa ushahidi?

“Hata leo ukienda TFF wakakupa barua kwamba hii barua tuliyoletewa ni feki nipo tayari kuthibisha lakini katika press conference zote zilizotolewa nimeziangalia TFF hawajaonesha barua wanayoilalamikia sasa mimi nakubali au kukataa barua ipi? Ila ninachokubali ni kwamba nilikuwa mkurugenzi katika kampuni aliyoiendesha marehem lakni hiyo barua wanayolalamika imefojiwa naomba wailetwe kwanu mimi nipo tayari kuja kuiona halafu nithibitishe ndiyo au hapana.

Baada ya kufariki mkurugenzi mtendaji tulitangaza kampuni inasimamisha shughuli zake zote mpaka itakapotangazwa vinginevyo.

Shaffih Dauda amchana Nyamlani “Usituchafulie taasisi”

$
0
0

Story kubwa kwenye soka la bongo kwa sasa ni kuhusu uteuzi wa Athumani Nyamlani kuwa makamu wa Rais wa TFF ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi baada ya Michael Wambura kufungiwa maisha kujihusisha na shughuli za soka kufuatia kukutwa na hatika katika tuhuma tatu tofauti zilizokuwa zinamkabili.

Ishu ya uteuzi wa Nyamlani bado haijatangazwa rasmi na TFF, lakini vyanzo vya ndani ya shirikisho hilo la soka tayari vimesha ‘nyapianyapia’ na kutoa ubuyu kwamba Nyamlani ndiye makamu mpya wa Rais wa TFF.

Shaffih Dauda alianza kutofautiana na uteuzi huo mara moja baada ya taarifa hizo kuvuja na kuanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, Machi 25, 2018 Dauda kupitia ukurasa wake wa Instagram ali-post ujumbe kumpinga Nyamlani.

“Sitaki kuwa mnafiki bro you don’t deserve kuwa makamu wa raisi wa TFF, katika hili natofautiana na Rais Karia,nina sababu zaidi ya milioni moja why hafai.”

Picha halikuishia hapo, baadae akaangusha tena post ya nguvu ambayo imeeleza baadhi ya sababu za kumpinga nyamlani kuwa makamu wa TFF.

“Nyamlani sikilza sauti za wapenda soka na urudi ukasome article 50-1 katika msahafu wa maadili ya TFF.”

“TFF ni taasisi ya umma yenye misingi ya maadili na utawala bora (good governance) haiwezi kutumika kama kichaka chako cha kujifichia.”

“Tanzania inajua ulipotoka umeondolewa kwa ukosefu wa maadili (integrity) katika chombo cha umma chenye hadhi ya juu sana nchini mahakama.”

“Mwerevu asingekubali hata kuwa mjumbe wa kuteuliwa wa kamati ya utendaji TFF, ukiachilia mbali hiyo ya kuwa makamu wa Rais cheo cha pili kwa ukubwa ndani ya TFF.”

“Katika kanuni za maadili, uadilifu ni dhima ya juukabisa katika kada yoyote ile duniani. Leo hii kuna watu hatunao tena katika medani ya soka kwa kukosa uadilifu (integrity), iweje wewe unarudi huku?

“Tunaomba ukae pembeni usituchafulie taasisi na watu tuliowachagua kwa umakini mkubwa. “A questionable integrity is a serious problem.”

Niyonzima amerudi Simba

$
0
0

Kiungo wa Simba Haruna Niyonzima ameanza mazoezi na wenzake baada ya kuwa nje kwa muda mrefu akiuguza majeraha. Niyonzima alikwenda india kwa ajili ya matibabu ambapo ilielezwa angefanyiwa upasuaji mdogo lakini jambo zuri ni kwamba alitibiwa bila kufanyiwa upasuaji.

Niyonzima anaamini baada ya muda mfupi atarudi uwanjani baada ya kumaliza program za mwalimu.

“Siwezi kuja mazoezini kabla sijawa vizuri, lakini siwezi kuesema nipo vizuri kwa 100% watau wanachotakiwa kujua, mtu ukitoka kwenye maumivu huwezi kuja kujiunga na timu moja kwa moja lakini ninachoshukuru naona kama napiga hatua kwa sababu siku za nyuma nilikuwa nyumbani lakini sasa nimeanza kuungana na timu.”

“Kwa sasa najisikia nafuu na nimeanza kupewa ratiba na mwalimu naamini mambo yatakuwa mazuri. Kuna ‘recover’ za ina mbili kuna ya daktari na mwalimu, ya daktari tayari nimeshafanya sasa hivi nafanya ya mwalimu kwa hiyo ikiisha najiunga na timu.”

“Nimemi-miss kucheza kwa sababu muda mrefu sijacheza na watu wanajua mpira ni kazi yangu lakini siwezi kuchukua uamuzi nikasema nacheza, natakiwa kwenda na ratiba ya timu, daktari na mwalimu lakini sasa hivi nipo kwenye ratiba ya mwalimu, muda si mrefu nitarudi uwanjani.”

Viewing all 565 articles
Browse latest View live