Na Baraka Mbolembole
OBREY Chirwa amefunga goli lake la 11 msimu huu katika ligi kuu Tanzania Bara (goli moja pungufu ya yale aliyofunga katika msimu wake wa kwanza akiichezea Yanga SC).
Raia huyu wa Zambia amekuwa na habari nyingi tofauti tangu aliposajiliwa kutoka FC Platinum ya Zimbabwe, Juni 2016. Chirwa alitajwa kama mchezaji mwenye thamani kubwa zaidi katika soka la Tanzania baada ya kusajiliwa kwa kiasi kinachosemekana milioni 200 za Kitanzania.
Kama hiyo ndiyo bei yake iliyomleta ‘Jangwani’ hapana shaka yoyote kuwa anaendelea kubaki mchezaji ghali zaidi nchini. Kama sivyo ni nani sasa?
Muda
Chirwa alichukua muda mrefu sana kueleweka kiuchezaji ndani ya kikosi cha Yanga. Ujio wake ulivuruga mahusiano ya kimpira kati ya washambuliaji nyota wa Yanga, Mrundi Amis Tambwe na Mzimbabwe Donald Ngoma ambao kwa pamoja waliifungia Yanga jumla ya magoli 38 katika ligi kuu msimu wao wa kwanza wakicheza-pacha-2015/16.
Wakati timu ikiwa katika maandalizi ya msimu mpya na michuano ya makundi Caf Confederation Cup huko Uturuki, Ngoma na Tambwe walifikia hatua ya kutaka kupigana kufuatia Mzimbabwe huyo kumkebehi Tambwe na kumwambia ‘mwisho wako wa kutamba umefika.’
Ngoma na Chirwa walicheza pamoja huko Zimbabwe hivyo ujio wa Mzambia huyo katika kikosi cha Yanga kwake ulikuwa ni zaidi ya sababu za kimpira-urafiki pia ukihusishwa. Ndani ya uwanja alipoanza kucheza tu akiwa na jezi ya Yanga, Chirwa hakuonyesha kiwango kizuri kama mshambuliaji aliyesajiliwa kwa ajili ya kufunga magoli.
Alionekana ni mchezaji mzuri katika kumiliki mpira, kushambulia akitokea pembeni huku akitengeneza nafasi na kupiga pasi za magoli kwa wenzake. Hii haikuwa kazi aliyoletwa kuifanya Yanga ndio maana hata upande wangu niliamini awali mchezaji huyo ni ‘hasara’ katika kikosi ambacho tayari kilikuwa na wachezesha timu wengi.
Siku zote ‘muda’ huamua, na ndicho kilichokuja kutokea. Majeraha ya Donald Ngoma yalipomuanza msimu uliopita, Chirwa akaanza kupata nafasi ya kucheza sambamba na Tambwe katika safu ya mashambulizi. Akaanza kufunga vs Toto Africans, akafunga tena mara mbili katika ushindi wa Yanga 6-2 Kagera Sugar FC katika uwanja wa Kaitaba.
Kufunga kwake magoli manne katika michezo miwili ya Kanda ya Ziwa kulianza ‘kumsafisha’-kutoka katika ‘garasa’ na kuumia kwa Tambwe kulimfanya Chirwa apewe nafasi zaidi ya kucheza kama mshambulizi ambaye timu inamtegemea kufunga magoli.
Ushirikiano wake na Saimon Msuva ambaye alikuja kutwaa tuzo binafsi ya ufungaji bora mwishoni mwa msimu uliisaidia mno Yanga kutetea ubingwa wake kwa mara ya tatu mfululizo.
Namna alivyokuwa akicheza kwa kujituma baada ya kuaminiwa kwa kweli kulinifanya nigeuze maneno yangu na mara baada ya kufunga goli pekee la juhudi binafsi vs Azam FC nilisema ‘huyu Chirwa ni shujaa wa Yanga msimu huu’ hadi sasa naamini kitendo cha Yanga ‘iliyokosa makali’ kuishinda Azam FC 1-0 Aprili mwaka jana ndiyo kiliipa taji.
Katika soka ili upate mataji unalazimika kushinda michezo yako kabla ya kutegemea kushindwa kwa timu nyingine na ndicho walichofanya Yanga msimu uliopita hata kama kuna timu ziliwasaidia kwa kuifunga Simba waliokuwa wakishindana nao.
Chirwa alimaliza msimu wake wa kwanza akiwa amefunga magoli 12 katika VPL, matano katika FA cup.
Amepandisha thamani yake, ila hajafikia milioni 200
Kufunga magoli 12 kwa msimu kwa mchezaji aliyesajiliwa kwa lengo la kuifungia timu magoli si ‘haba’ hasa ukizingatia mchezaji mwenyewe ndiyo kwanza alikuwa akicheza Tanzania kwa mara ya kwanza, lakini kwa aina ya kiwango chake hadi sasa ni wazi Yanga ilikosea kumsaini kwa thamani ile kubwa.
Ndiyo alisaidia mno kuipa ubingwa msimu uliopita lakini ndani ya kikosi chao mchezaji aliyepaswa kuwa na thamani kubwa ni Msuva. Si kwasababu alishinda tuzo ya ufungaji bora , hapana, ni kwa sababu alionyesha yuko tayari wakati wote kuibeba timu yake hata wakati ikiwa katika ‘anguko la kiuchumi.’
Chirwa ameendelea kuwa na maendeleo mazuri kimpira ndani ya Yanga lakini nje ya uwanja ni mchezaji ambaye anapaswa kujitazama pia na kujithaminisha kama kweli anastahili kuwa mchezaji ghali zaidi wa klabu na katika soka la Tanzania.
Ameshafunga ‘hat-trick’ mbili msimu huu (mchezaji pekee kufanya hivyo msimu huu katika VPL hadi sasa), magoli 11 katika mzunguko wa 18 wa ligi, pia akiwa ameshakosa michezo sita kutokana na kufungiwa (mitatu mwanzoni mwa msimu kutokana na makosa aliyofanya katika mchezo wa mwisho msimu uliopita vs Mbao, na mingine mitatu alifungiwa Desemba-Januari).
Pia kuna michezo kama miwili alikosa kutokana na majeraha. Ukitazama vizuri idadi ya michezo aliyocheza katika ligi na idadi yake ya magoli utagundua kuwa Chirwa ametengeneza wastani wa kufuga goli moja kila mechi.
Lakini je hii inatosha kumfanya mchezaji huyo asajiliwe tena Yanga kwa thamani ya zaidi ya ile aliyoingilia? Upande wangu, hapana lakini kuelekea miezi yake minne iliyosalia katika mkataba wa sasa anaweza kuwashawishi watu wakampatia anachotaka.
Ila akumbushwe
Hakuna mchezaji aliyetoka Yanga moja kwa moja na kwenda kupata mafanikio Simba zaidi ya Mohamed Banka ambaye pia alisajiliwa Simba kama mchezaji huru baada ya kumalizika kwa mkataba wake Yanga na kunyimwa mpya katikati ya mwaka 2008.
Haruna Niyonzima ni mfano tu ambao anaweza kuutazama, japo Mnyarwanda huyo hawezi kuondoka mioyoni mwa wanayanga lakini alishapoteza nafasi ya kuwa mfalme klabuni hapo japo alifanikiwa kwa misimu sita aliyokuwa hapo.
Chirwa anapaswa kucheza zaidi na kuisaidia Yanga wakati huu wakipambana na kikosi chenye majeruhi wengi kutetea nafasi zao za uwakilishi Caf mwaka ujao. Kama Yanga itashindwa kufuzu kwa michuano ya Caf msimu ujao ni wazi thamani za wachezaji zitashuka tofauti na kama ikitokea wakafuzu.
Huu ni wakati wa mchezaji huyo wa Zambia kujiuliza kama kweli amelipa walau nusu ya milioni 200 ambayo analazimishwa kumaliziwa hivi sasa? Hata kama Yanga haitampa sasa, pesa yake itamfikia kwa maana ipo katika makubaliano rasmi, ila kuendelea ‘kususa-susa’ kucheza wakati huu hakusaidii klabu wala yeye mwenyewe, na kitendo cha kuwaza kuhusu Simba hivi sasa ni dhaifu ambalo linaweza kumuangamiza.
Miezi minne iliyobaki katika mkataba wa Chirwa na Yanga inaweza kuwa na thamani kubwa klabuni na kwa mchezaji mwenyewe kama atatuliza akili yake wakati huu uongozi ukipambana kuakikisha matatizo ya wachezaji yanatatuliwa.
Chirwa anaweza kutengeneza ufalme na maisha ndani ya Yanga maana shida za klabu zetu hizi zinatafutiwa ufumbuzi kuelekea mifumo mipya ya kiuendeshaji. Mwambieni, Chira ukipata kilicho bora Yanga ni ngumu kukikuta Simba, Niyonzima ni mfano tu, uhalisia tunaufahamu.
Afanye kazi ya mwajiri wake wa sasa na kuachana na mawazo ya kule anapotaka kwenda. Ataenda muda ukifika.