Wakati Farid Musa anaondoka jana December 28 kwenda Hispania kujiunga na timu ya Tenerife ni siku hiyohiyo ambapo benchi la ufundi la Azam FC likiongozwa na kocha mkuu Zeben Hernandez lilifutwa kazi.
Farid Musa amesema kitu ambacho alikuwa akishauriwa na aliyekuwa kocha mkuu wa Azam FC Zeben Hernanez. Farid ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Tanzania amesema, Zeben alikuwa akimsisitiza kama atajituma na kuwa na nidhamu basi atafika mbali zaidi ya Tenerife.
“Ukiendelea kujituma hivyohivyo na nidhamu utafika mbali sio Tenerife tu. Na yeye ni kati ya watu waliokuwa wana-push mimi niondoke na alikuwa anaumizwa kuona mimi nakaa nje na naendelea kuwepo Tanzania,” alisema Farid Muda mfupi kabla ya kuondoka Dar es Salaam.
“Naomba watanzania wawe na subira kwa sababu naenda kuanza upya, sijacheza mechi kwa muda mrefu nilikuwa nafanya tu mazoezi.”
Hakuna kiongozi yeyote wa Azam aliyemsindikiza Farid uwanja wa ndege wa kimataifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere lakini Farid alisema hakuna tatizo katika hilo na haliathiri kitu chochote katika safari yake.