Na Abubakar Khatib ‘Kisandu’, Zanzibar
Jana Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limepanga Draw ya mechi za awali kuwania taji la ligi ya mabingwa Afrika pamoja na kombe la Shirikisho, Wawakilishi wa Zanzibar kwa upande wa kombe la Klabu Bingwa timu ya Zimamoto imepangwa kucheza na Ferroviario Beira ya Msubiji huku wenzao KVZ ambao wanawakilisha Zanzibar katika kombe la Shirikisho imepangwa na Messager Ngozi ya Burundi.
Kocha Mkuu wa KVZ Abdulghan Msoma amekiri kuwa mchezo huo utakuwa mgumu dhidi ya Messager Ngozi ya Burundi lakini amejipa matumaini kwa kusema kuwa watapata mazoezi mazuri katika mashindano ya Mapinduzi.
“Ratiba nimeipata lakini nakiri kuwa si timu mbovu Messager Ngozi, lakini muda upo tunazidi kujiandaa na pia Mashindano ya Mapinduzi yatatusaidia kupata mazoezi kwa sababu tutakutana na timu kama URA ya Uganda na Simba, japo kuwa kombe la Mapinduzi pia ni mashindano lakini yatatusaidia huko CAF, sasa naamini kuwa tutapata mazoezi mazuri lakini wa Burundi si timu mbovu nawajua vyema wale”, amesema Msoma.
Kwa upande wake Ali Ussi Bakar ‘Jongo’ ambae ni katibu wa timu ya Zimamoto ambao wanawakilisha Zanzibar katika mashindano ya kombe la klabu bingwa Barani Afrika ambapo Zimamoto watacheza na Ferroviario Beira ya Msubiji, Jongo kwanza ameshukuru kunusurika kukutana na timu kutoka nchi za Kiarabu ambapo amesema watapambana na Ferroviario Beira ya Msubiji kwani kwasasa wapo katika maandalizi makali ya mwisho mwisho.
“Kama unavyoona hapa tupo mazoezini tunajiandaa na Ferroviario Beira ya Msubiji, lakini ni game ngumu kwani nasikia jamaa si wabaya, ila sisi tumeshukuru kwakuwa hatuchezi na timu za Kiarabu, kwaiyo tutapambana ili tutinge raundi inayofata,” amesema Jongo.
Mechi za hatua ya awali zinatarajiwa kuchezwa February 10,11 na 12 2017 huku zile za marudiano zikitaraji kupigwa March 17,18 na 19, 2017 ambapo Zimamoto na KVZ wote wanaanzia nyumbani uwanja wa Amaan, Zanzibar.