
Na Baraka Mbolembole
KUFUATIA ‘mizengwe’ anayoifanya mmiliki wa African Lyon, Rahim Zamunda kwa wachezaji Waganda, Tito Okello na Hood Mayanja ambao wapo huru lakini bosi huyo ana wang’ang’ania baada ya kusikia timu ya Mbeya City FC inataka kuwasaini katika dirisha hili dogo la usajili, baadhi ya wachezaji wa zamani katika soka la Tanzania nao wameibuka na kusema yao.
“Bongo mpira mufilisi” ameandika Patrick Mrope mchezaji wa zamani wa Ashanti United na Stand United.
“Mpira wa kibongo ni kukomoana tu ndio kumezidi. Na hawa watu wenye ‘hela uchwara’ wakati mwingine wana haribu fani zetu kwa maamuzi yao wanayotaka.” anasema mshambulizi wa zamani wa Serengeti Boys, Taifa Stars na klabu ya Mtibwa Sugar, Omar Matutta.
“Hapo ndipo ninapochoka na viongozi wetu magumashi katika soka letu. Wachezaji si wamemaliza majukumu yao Lyon, nini tena wahitaji? Kipindi chetu viongozi wanakuacha usajili umeshafungwa na kukwambia mapema ya kwamba hawakuitaji ni dhambi kwao sielewi kwa nni viongozi wa soka wanakuwaga na roho mbaya sana.” anasema na kuhoji mlinzi wa zamani wa Taifa Stars ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kilichofuzu 8 bora kwa mara ya kwanza katika Caf Champions League 1998, Mzee Abdallah Ngaunja.
“Dah! mimi siwezi kumshangaa sana mshikaji (Zamunda) ana kawaida ya majivuno, jeuri na kuwadharau wachezaji na anachokitaka yeye ndiyo hivyohivyo anataka kiwe. “
“Nakumbuka mpira niliacha kucheza nikiwa Lyon kama miaka 6 au 7 iliyopita tena ikiwa imebakiza kama mechi tano za ligi imalizike. Niliona napoelekea ningemkunja mtu. Nikionaga habari zake nakumbuka alafu naishia kupata maumivu.” anasema mlinzi wa zamani wa APR, Yanga SC na timu ya Taifa, Hamis Yusuph ‘Waziri wa Ulinzi’