
Na Baraka Mbolembole
KUANZIA wiki hii nitakuwa nikiwaletea kolamu ya wachezaji wa zamani katika soka la Tanzania ‘MWANASOKA ALIYEPITA.’
Leo nimeanza na mlinzi wa zamani wa Zaragoza United, Mseto FC, Reli FC, Simba SC na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars,’ Fikiri Magosso ambaye sasa anaendesha maisha yake akiwa maeneo ya Temeke, Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam.
shaffihdauda.co.tz: Ulicheza soka la ushindani kwa miaka mingapi katika ligi za juu?
Fikiri Magosso: Nilianza kucheza soka la ushindani yapata miaka ya 1985 hivi nikiwa Mkoani, Morogoro. Nilianzia kucheza soka nikiwa Zaragoza United (Moro United) timu hiyo ilikuwa ikimiliwa na Said Hafif, nakumbuka nilichezea United katika ligi daraja la tatu pale Morogoro miaka ya 1986 na 1987, kisha nikasajiliwa na mabingwa wa zamani wa Tanzania Bara timu ya Mseto FC.
Baada ya kuichezea Mseto kwa muda mfupi nikachaguliwa katika kikosi cha timu ya Mkoa wa Morogoro ‘Moro Stars’ ambayo ilishiriki katika michuano ya kombe la Taifa ‘Taifa Cup’ mwaka 1988.
Baada ya kumalizika kwa michuano ile nikasajiliwa na Reli FC ‘Kiboko ya Vigogo’ pia ya Morogoro na ni hapo nilipoanza kupata mafanikio zaidi kwa sababu nilipata nafasi ya kuteuliwa katika timu ya Taifa ya vijana kwa mara ya kwanza.
Baada ya kuichezea Reli kwa miaka miwili nikajiunga na Simba SC mwaka 1990 na nilicheza kwa miaka minne katika timu hiyo hadi kustaafu kwangu kutokana na kushindwa kupona maumivu ya goti ambayo yalisababisha nikafanyiwa upasuaji mara mbili.
shaffihdauda.co.tz: Nasikia ulikuwa beki mahiri wa kati. Nafasi gani ulipendelea kucheza?
Fikiri Magosso: Nikiwa Zaragoza United, Mseto FC nilikuwa nikicheza nafasi ya kiungo wa ulinzi-namba 6. Nilipohamia Reli FC, Mkufunzi, John Simkoko akawa ananichezesha nafasi tofauti tofauti (namba 6, 8, 4 na 5). Nafasi za beki wa kati nilizimudu vyema na nilizitumikia hadi nilipostaafu mwaka 1994.
shaffihdauda.co.tz: Ni mataji mangapi ulipata kushinda?
Fikiri Magosso: Nimeshinda mataji mengi wakati wangu wa uchezaji. Nilishinda ubingwa wa Mkoa wa Morogoro mara mbili nikiwa na Mseto FC miaka za 1986 na 1987. Nilishinda mataji mawili ya Shimuta 1988 na 1989 nikiwa na timu ya Reli FC.
Nimeshinda Cecafa Kagame Cup mara moja nikiwa Simba SC mwaka 1991, nilishinda taji lingine moja la Hedex Cup nikiwa Simba mwaka 1992, nilikuwa sehemu ya timu ya Simba ambayo ilimaliza katika nafasi ya pili katika ligi kuu ya Muungano mwaka 1992 na michuano ya Caf Confederation Cup mwaka 1993.
shaffihdauda.co.tz: Kitu gani unakumbuka katika mafanikio yako kiuchezaji wakati huo?
Fikiri Magosso: Kikubwa ni kuijua dunia, kufahamiana na watu na mambo mengine ya kawaida tu. Kama unavyojua wakati sisi tunacheza tulikuwa tukiongozwa na mapenzi tu ya mchezo wenyewe huku tukiwategemea sana wafadhili na si mishahara.
Mafanikio mengine naomba iwe siri yangu, maana siwezi kuzungumzia vitu vidogo vidogo nikasema ni mafanikio makubwa kwangu.
shaffihdauda.co.tz: Ulicheza Simba kwa miaka minne, kitu gani unakikumbuka hadi sasa ukiwa nje ya timu?
Fikiri Magosso: Timu ya Simba niliyochezea mimi ilikuwa na ubora, nidhamu, ushirikiano, upendo na uanamichezo. Nakumbuka mwaka 1993 tulikosa ubingwa wa Caf (sasa Caf Confederation Cup) baada ya kupoteza 2-0 nyumbani dhidi ya Stella ya Ivory Coast katika mchezo wa fainali ya pili. Matokeo ya awali yalikuwa 0-0.
Kwa kweli nilipatwa na ‘machungu’ baada ya mchezo kumalizika. Magoli tuliyofungwa yalikuwa ni ya kizembe sana. Sitaki kusema sana kuhusu yaliyotokea, lakini kulikuwa na hujuma.
Nilishazungumza sana siku za nyuma sasa sipendi nigombane na ndugu zangu. Kama tungepata ushindi na kutwaa ubingwa ule kila mchezaji aliahidi kupewa Toyota Corola.
shaffihdauda.co.tz: Nimekuelewa kaka. Mwaka 1994 nakumbuka Simba iliifunga Yanga magoli 4-1, nilikuwa na miaka 8 wakati huo lakini nakumbuka mara baada ya kumalizika kwa mchezo ule mashabiki wengi wa Simba waliingia barabarani kushangilia ushindi ule.
Walitoka CCM Mahenge, Ulanga hadi maeneo ya Kwiro Sekondari na kurejea nyumbani. Miaka 22 sasa imepita, hamasa ile haipo tena kwa mashabiki? Unadhani ni kwanini hamasa imeshuka sana?
Fikiri Magosso: Simba na Yanga ni ‘watani wa jadi,’ Simba na Yanga ni ‘wapinzani wa jadi.’ Watanzania wote wanaopenda mpira wa miguu hizi ndiyo timu zao za zamani na hadi sasa wanazipenda. Wakati sisi tunacheza hadi wachezaji wenyewe walikuwa wakizichezea kwa sababu ya mapenzi zaidi kwa timu yake lakini hilo kwa sasa halipo.
Naweza kusema mpira wetu umepoteza ladha kidogo. Hivi sasa walimu na wachezaji wanashindwa kutengeneza matokeo kiwanjani badala yake viongozi wanawavuruga waamuzi ili wapate matokeo ndani ya uwanja.
Hiyo inasababisha mashabiki kubaki wakilaumu zaidi kuliko kufurahi. Zamani utani wa timu hizi ulifikia watu kuweka ‘bondi’ nyumba, gari au mke lakini sasa hivi ni matusi tu.
shaffihdauda.co.tz: Ukitazama wachezaji wa zamani na sasa, tofauti yao ni ipi hasa?
Fikiri Magosso: Tofauti ipo kubwa tu, Kwanza wachezaji wa zamani walikuwa ‘wanajua sana’ na walitapakaa nchi nzima. Pili walikuwa na miili mikubwa ‘ya kutisha’, Tatu, ilikuwa ukiitwa katika timu ya Taifa lazima ustuke na kujiuliza ni ‘mimi au wamekosea jina.’
Kumbuka Simba ilifika fainali ya Caf mwaka 1993 pasipo kuwa na mchezaji yeyote wa kulipwa katika kikosi. Yanga ilishinda Cecafa Kagame Cup mwaka 1993-Uganda bila kuwa na mchezaji yeyote wa kigeni katika timu yao, lakini leo ukitazama ligi ya Tanzania Bara imejaa wachezaji wa kulipwa kutoka nje ya nchi.
Hivi sasa dirisha dogo la usajili liko wazi ila hakuna mchezaji yoyote yule kivutio anayezungumzwa kusajiliwa na Yanga au Simba.
Nakumbuka mwaka 1988, Hamis Gagarino (mwenyezi Mungu amrehemu), Zamoyoni Mogela, Lilla Shomari, James Kisaka walikuwa wakicheza Volcano ya Kenya na walikuwa na msaada mkubwa hadi katika timu yetu ya Taifa. Lakini angalia sasa Taifa Stars hakuna ushindi wakati sasa kuna hali nzuri kiuchumi.
shaffihdauda.co.tz: Kwanini hata nyakati zenu Tanzania haikufanikiwa kucheza AFCON wala kukaribia kufuzu kwa kombe la dunia wakati mlikuwa na uwezo mkubwa kiuchezaji?
Fikiri Magosso: Mfumo wa zamani haukuwa mzuri sana, hata timu ya Taifa haikuwa ikipewa kipaumbele sana kama ilivyo sasa. Watu walikuwa wanajali zaidi Simba na Yanga, timu ya Taifa ilikuwa ikiweka kambi sehemu kama ‘salvation army’ na haikuwa na udhamini. Mifumo ilikuwa ya hovyo na ndio sababu kubwa ya kutofanikiwa wakati wetu.
shaffihdauda.co.tz: Kama ungekuwa katika nafasi ya uongozi Simba SC ungefanya kitu gani ili kuisaidia klabu kimpira na kiuchumi?
Fikiri Magosso: Mpira ni pesa, bila pesa hakuna mpira. Ningekuwa katika nafasi ya uongozi Simba ningeiweka timu katika kambi nzuri, ningelipa mishahara mizuri kwa wachezaji na walimu, ningetoa posho zao kwa wakati lakini hayo yote utekelezaji wake unataka pesa hivyo ningetafuta wadhamini na kuingia nao mikataba yenye maslai kwa klabu na si watu binafsi.
shaffihdauda.co.tz: Wito wako ni upi kwa wadau wote wa mpira kwa sasa?
Fikiri Magosso: Tushikamane kuhakikisha Tanzania tunapiga hatua tutoke hapa tulipo. Tuache kuwalaumu viongozi, tuwape ushauri pale penye mapungufu, wenzetu Uganda angalau leo wanavaa jezi ya Taifa lao na kutembea kifua mbele. Tuwekeze katika soka la vijana na turudishe soka mashuleni, pia turudishe Taifa Cup. Tuipende timu yetu ya Taifa.