
Kocha wa timu ya taifa ya kuogelea ya Tanzania Alexander Mwaipasi ameieleza shaffihdauda.co.tz changamoto kadhaa ambazo wamekuwa wakikutana nazo wao kama timu lakini pia kama wadau wa chama cha kuogelea ambazo zimekuwa zikiwafanya washindwe kuwaandaa vizuri vijana kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye mashindano.
Kocha huyo anasema Tanzania kama nchi haina bwawa hata moja ambalo linawapa fursa wachezaji wa mchezo huo kufanya mazoezi badala yake wamekuwa wakiomba sehemu mbalimbali na wanapokataliwa maana yake mazoezi hakuna.
Kama mwalimu wa mchezo wa kuogelea, vijana wetu wamefanya vizuri sana. Binti kaogelea vizuri sana, simsifii tu lakini nazungumza kutokana na mazingira ya maandalizi yetu na huyu wa kiume kafanya vizuri zaidi kutokana na mazingira yake aliyokuwa akifanya mazoezi.
Tupo kwenye mchezo wa kuogelea lakini watu tunaoshindana nao hakuna ulinganifu hata kidogo. Mfano mdogo ni kwamba, umeenda kwenye mashindano ya baskeli wakati wewe unafanyia mazoezi baskeli ya Swala huku wenzako wanafanyia mazoezi zile zitakazotumika kwenye mashindano halafu wewe unaenda kukutana na baskeli ya mashindano baada ya kufika kwenye mashindano yenyewe.
Kwa kifupi nchi yetu haina bwawa hata moja, achana na kwamba chama chetu cha kuogelea kinalilia bwawa la mita 50 lakini hakuna bwawa lolote. Kwahiyo mabwawa ambayo tunatumia ni ya kuombaomba, wenye mabwawa wakiruhusu mnafanya mazoezi wakisema linashughuli nyingine mnaacha.
Mchezo wa kuogelea ni miongoni mwa michezo mitatu migumu duniani, na hii ni mara ya tatu Tanzania kama nchi tunashiriki michuano ya kuogelea. Hata kama tutapata bwawa lakini hili jambo lisichukuliwe kichama lichukuliwe kwa namna ya nchi. Lazima zitengenezwe sera za nchi kwa maana kuanzia serikali ya juu.
Kama utapata nafasi ya kuhoji nchi zote zilizoleta waogeleaji wao angalia namna walivyowekeza kwenye michezo, sisi kama tungekuwa tumewekeza halafu tunarudi mikono mitupu nyumbani nadhani tungefia njiani hata nyumbani tusingeingia. Lakini hakuna mtu anayetudai na mimi najivunia performance ya vijana wangu lakini hatudaiwi kitu na mtu yeyote wala serikali haitudai kwasababu hadi tunafika hapa ni jitihada binafsi lakini sisi tulichobeba ni jina la Tanzania tu.