Kauzu FC imetinga fainali ya michuano ya Sports Extra Ndondo Cup baada ya kuichapa Misosi FC kwa changamoto ya mikwaju ya penati.
Mchezo huo wa nusu fainali ya pili ulipigwa kwenye uwanja wa Bandari ambapo ilishuhudiwa dakika 90 zikimalizika huku timu zote zikiwa hazijafungana na kuingia moja kwa moja kwenye changamoto ya penati.
Penati 5 za kwanza kila timu ilipata zote, wapigaji wakionesha ufundi wa hali ya juu katika kufunga kiki zao huku magolikipa wakijitahidi kuzuia mikwaju hiyo iziguse nyavu lakini wakashindwa kufanikiwa.
Katika hatua ya piga-nikupige kauzu walifunga penati mbili wakati Misosi wao walifunga moja na penati nyingine ikaokolewa na golikipa wa Kauzu FC.
Fainali ya pili ikaamuliwa kwa matuta baada ya Temeke Market pia kuitoa Makumba kwa changamoto ya mikwaju ya penati kwenye mchezo wao wa Jumamosi Julai 23.
Fainali ya Ndondo inatarajiwa kupigwa Julai 30 palepale kwenye uwanja wa Bandari, watoto wa Temeke wao wanauita Wembley.